Lady Jaydee yamemkuta


MWANAMUZIKI Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, juzi Jumatatu hatimaye yalimkuta baada ya kuibua simanzi nzito katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar, alipofikishwa baada ya kufunguliwa kesi ya madai namba 29/2013 na mabosi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga.

KAMA JAY-Z NA BEYONCE
Hali katika mahakama hiyo iligubikwa na huzuni baada ya watu kumuona Lady Jaydee akiwasili eneo hilo sambamba na mumewe Gadner G Habash ambapo walifananishwa na wanandoa mastaa wa Marekani, Shawn Carter ‘Jay Z’ na Beyonce Giselle Knowles, walipotimba mishale ya saa 6:00 mchana.
Risasi Mchanganyiko liliwashuhudia mastaa hao wakiingia eneo hilo huku wakiwekewa ulinzi mkali kama ilivyo kawaida mahakamani kuhakikisha usalama wa watu.
Wawili hao waliongozana hadi chumba cha makarani ambapo walielezwa kesi inayomkabili mwanamuziki huyo na kupangiwa siku ya kesi ambayo ni Mei 27, mwaka huu.
Pia walitajiwa hakimu atakayeendesha kesi yao kuwa ni Athumani Nyamrani wa chumba namba 2 cha mahakama hiyo.
Baada ya kupewa utaratibu wa kesi hiyo walichomoka mahakamani na ndipo wakakutana na paparazi wetu aliyewasimamisha na kutaka kujua madai yaliyofunguliwa.