Jana hali ilikuwa tete huko Tunduma

Hali ilivyokuwa katika baadhi ya maeneo ya Tunduma leo (picha: Rashid Mkwinda)
Taarifa  kutoka Mbeya zinaripoti kutokea vurugu huko Tunduma zilizosababisha mtu mmoja kujeruhiwa, kutokana na mchanganyiko wa masuala ya kiimani katika uchinjaji wanyama baina ya Wakristo na Waislam na kwa upande mwingine “wapiga debe” waliochochea kukuza mambo kwa sababu wanazozijua wenyewe.

Mwandishi  wa habari aliyeko eneo hilo, Moses Ng'wat ameieleza blog ya blogu ya FrancisGodwin kuwa  vurugu  hizo zilianza  majira ya saa 4 asubuhi  kwa makundi  ya vijana  kuandamana mitaani na kuvutana  kuhusu uamuzi  wa viongozi  wa dini ya Kikristo, Tunduma  kuandika barua kwa mkuu  wa Wilaya ya kutaka  kuruhusiwa kuchinja  wakati wa sikukuu ya Psaka.

Alisema  kuwa kabla ya siku ya Ijumaa Kuu,  viongozi hao  wa dini ya Kikristo  walikutana na Mkuu  wa  Wilaya  ya Momba, Abood Saibea ambaye  aliwataka kuwasilisha barua rasmi .

Uchinjaji ulifanyika  siku ya Pasaka na hapakuwa na mvutano  wowote baada ya Wakristo kuchinja katika bucha zao na  Waislamu kuchinja katika bucha zao na kila mmoja  kufanya biashara  kwa kupata  wateja wake kama kawaida.

Lakini katika hali ya kushangaza, leo kuliibuka kundi la vijana wanaofanya kazi katika stendi na vijiwe mbalimbali, na kuanzisha vurugu kiasi cha kuwalazimu Polisi wa FFU kuingilia kati kwa kutumia mabomu ya machozi na kuwatawanya  wananchi  waliokuwa wamekusanyika maeneo mbali mbali.

Kutokana na vurugu  hizo mpaka  wa Tunduma  ambao unaingia nchi  za kusini  wa Tanzania  ulifungwa. Magari yaliyokuwa yakitoka  Sumbawanga  pia yalizuiwa kuendelea na  safari kwa muda hadi hali ilipotengamaa majira ya saa 8 mchana pale kamanda wa polisi wa mkoa  wa Mbeya  Diwani Athuman  alipofika katika eneo hilo.

Kwa ujumla inaripotiwa kuwa hakuna madhara makubwa yaliyotokana na vurugu hizo.

---
Hii ni taarifa za awali tu kadiri zinavyoripotiwa na walioko kwenye eneo. Ikipatikana taarifa rasmi, itawekwa hapa kama “update/taarifa mpya”. Tafadhali fuatiliakwenye  vyombo vya habari rasmi kwa taarifa sahihi kadiri zitakavyopatikana kutoka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyenye dhamana.