KUTOKA CCM MAKAO MAKUU::TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ijumaa iliyopita Mei 3, 2013 Msemaji wa kambi ya Upinzani Bungeni Masuala ya katiba na Sheria Ndg. Tundu Lissu katika hotuba yake pamoja na kuzishutumu taasisi zingine, lakini pia alitoa tuhuma kadhaa dhidi ya CCM.
Tuhuma hizo zilielekezwa kwenye maeneo kadhaa hasa yahusuyo suala la mchakato wa uundwaji wa katiba mpya unaoendelea nchini na ushiriki wa makundi tofauti katika mchakato huo.
Katika kuipa uzito hoja hiyo, Lissu alitoa malalamiko mengi dhidi ya CCM kwa madai kuwa tumeteka mchakato huo kwa kujaza Makada wa CCM katika Mabaraza ya Katiba yaliyoundwa kwenye ngazi ya kata hivi karibuni.
CCM Kama ilivyo taasisi yoyote makini na wenye uzalendo  kwa nchi yao, katika mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ina jukumu la kuwahamasisha wanachama na wasio wanachama wake kushiriki mchakato wa katiba nchini kutokana na kutambua umuhimu wake.
Tofauti ya CCM na Chadema katika hili ni,  wakati CCM tunahamasisha watu washiriki kwenye mchakato wa katiba nchini, Chadema wao wanahamasisha watu wavuruge au wasishiriki kabisa mchakato huu.
Mfano mzuri ni jitihada zao za kuziria mchakato huu kwa visingizio vya kitoto kabisa. Juhudi zao za kumtaka Prof. Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ambaye wao Chadema walimpendekeza kwenye tume, ajitoe kwenye tume zinafahamika na wala sio SIRI.
CCM inampongeza kwa dhati Prof. Baregu kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa aliouonyesha kwa kuwakatalia kujitoa kwenye tume na kuweka mbele masilahi ya taifa lake. Kukataa kwa Prof. Baregu kujitoa kwenye tume kwa hoja za kitoto kabisa za Chadema ilipaswa kuwa fundisho kwa vibaraka hawa.
Ilivyo fanya CCM, kuhamasisha wanachama na watanzania kwa ujumla kushiriki mchakato huo, ndivyo taasisi nyingine pia zilivyofanya. Zikiwemo taasisi za dini ambazo zimekuwa zikihamasisha zoezi hili kupitia mikusanyiko ya Ibada, Taasisi zisizo za Kiserikali yaani NGOs kwa kufanya makongamano na makundi mengine kwa kuendesha midahalo, dhambi kwa CCM inatoka wapi?.
Ifahamike kuwa mawasiliano na mjadala juu ya zoezi la mchakato wa uundwaji wa katiba mpya nchini hayakuanza jana ndani ya CCM, bali yalianza siku nyingi kwa  Chama kuunda kamati   iliyopitia na kuja na maoni ya CCM juu ya nini kiwemo kwenye katiba mpya.