Wizara yaendelea kusisitiza MSD iliuziwa ARV ‘feki
05:05
Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya ya Afya na Ustawi wa
Jamii imeendelea kusisitiza kwamba Kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari ya
Dawa (MSD) dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi aina ya TT-VIR 30
toleo Na.0C.01.85,kwa mujibu wa nyaraka zilizopo na kwamba dawa hizo
zilibainika kuwa ni bandia.
Msisitizo huo umetolewa katika vyombo vya habari
jana na ofisi ya Wizara ya afya na Ustawi wa jamii kupitia kwa msemaji
wake Nsachris Mwamwaja ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza
kwa wananchi.
Katika taarifa hiyo Serikali imesema kuwa kama
ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA kuhusiana na suala
hili, bado inasisitizwa dawa hizo zilikuwa bandia.
“Tunapenda kusisitiza kwamba, waziri katika hotuba
yake hakukanusha kuwa Kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali
alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika kiwanda cha kampuni hiyo
haukuonyesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd bali vifungashio ni vya
TPI Ltd na nyaraka zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo
bandia,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, msemaji huyo wa wizara katika taarifa hiyo
alieleza kuwa vyombo vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala
hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia .
Hivyo kwa kuzingatia unyeti wa suala hilo,wizara
imetoa wito kwa vyombo vya habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa
na vyombo vya usalama na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza
kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali katika kupambana na dawa
bandia nchini.
Mnamo Mei 9, 2013, Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Hussein Mwinyi katika kuhitimisha hoja ya bajeti ya wizara
alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja zilizokuwa
zimetolewa na Zarina Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa Kiwanda cha Dawa
cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa
bandia ya ARV.
Hata hivyo baada ya ufafanuzi huo wa waziri
kutolewa,kumekuwa na taarifa mbalimbali kupitia baadhi ya vyombo vya
habari zinazoleta mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala hilo hivyo
wizara imeamua kutoa ufafanuzi huo kwa jamii kwa lengo la kuondoa
mkanganyiko huo ulioanza kujitokeza.

0 comments:
Post a Comment