Maisha Feki ya Mastaa wengi wa Bongo
00:48
TASNIA ya muziki wa kizazi kipya Bongo kwa sasa imeshika kasi,
wasanii kwa kiasi kikubwa wameweza kuwekeza na hata majina yao yamekuwa
juu kiasi cha kujijengea imani kubwa mbele ya jamii.
Imani hii kubwa na ushabiki uliokithiri, imezua
jambo jingine kubwa ambalo limekuwa tatizo la kimaendeleo. Tatizo hilo
ni wasanii kujikuta wakiendeshwa na umaarufu wa majina yao katika namna
ya wanavyoishi.
Imebainika kwa kuwa majina yao ni makubwa kuliko
uwezo wao wa kuishi. Jambo hili limewafanya wasanii hao waishi maisha
feki mbele ya jamii yao.
Kwa kuishi maisha hayo, wamejikuta wakitumia gharama kubwa katika kuishi maisha ambayo si ya daraja lao.
Mavazi
Ukianzia na mavazi, kwa kuwa tu anajulikana yeye
ni yule msanii aliyeimba wimbo fulani maarufu, basi hata kama hana
mavazi ya gharama atajitahidi hata kwenda kuazima, ili mradi mashabiki
wake wakimwona wamkute nadhifu.
Awali tabia hiyo ilidhaniwa ni ya wasanii wa dansi pekee hasa Wakongomani, lakini sasa ni fasheni kwenye Bongofleva.
Inakubalika na ni dhahiri unadhifu kwa watu wenye
mvuto kwa jamii ni jambo lililo wazi, lakini unadhifu unahusiana vipi na
gharama?
Wengi wanapotelea hapa, wanafikiri unadhifu ni
kuvaa vitu vyenye gharama kumbe uchaguzi wa vitu vya kawaida na
mpangilio vinaweza kukufanya kuwa nadhifu kuliko vitu ghali.
Angalia mavazi ya Michael Jackson, yalikuwa ya
gharama sana lakini si kweli kwamba mavazi yale ndiyo yalikuwa
yakisababisha aonekane nadhifu kuliko wasanii wote duniani, alikuwa tu
ni Mfalme wa Pop.
Lakini Bongo ukiachilia mbali kuazimana, kuvaliana
na kuambukizana magonjwa, kuna kundi kubwa la wasanii ambao hupenda
kujihusisha na maduka ya nguo ili mradi tu wapate kupendeza.
Usafiri
Ukishakuwa staa, tayari kuitwaitwa barabarani, kufuatwa na
watoto ukiwa katika matembezi yako, ama kuombwa kupiga picha na
mashabiki wako na mambo mengineyo kama hayo ni jambo la kawaida.
Wasanii wetu wanahisi hii ni ghasia na kuwakimbia
mashabiki wao. Huukimbia kabisa usafiri wa umma, yaani daladala au
wakati wanaenda mikoani huona bora hata wakodi magari badala ya kupanda
basi.
Kuna asilimia kubwa ya wasanii tunaowaona
wanaendesha magari kana kwamba wanayamiliki, kumbe si yao. Wengi
huyakodi ili wakionana na mashabiki wao angalau waonekane wao ni wa
matawi ya juu.
Jina linaendelea kuwa kubwa huku mhusika akiteseka kwa kuingia madeni makubwa.
Amini usiamini humu ndimo asilimia kubwa ya kipato
cha msanii wa kizazi kipya kinapopotea. Magari hukodishwa kuanzia Dola
25 mpaka Dola 40 kwa siku kulingana na aina ya gari.
Makazi
Hapa ndipo ambapo hawajali kabisa, wengi wao
huishi kwa kutegemea wazazi na wengine huishi kwenye nyumba za kupanga
kwa kuchangia au kukaa tu kwa mtu huku wakiamini ipo siku mambo yatakuwa
sawa wajenge.
Nyumba wanazoishi wengi wao ukiangalia na mavazi
wanayovaa na magari wanayoendesha ni vitu tofauti. Wengi huweka
kipaumbele mwonekano wa nje kuliko hata wanapoweka ubavu.
Ni wasanii wachache wanaomudu maisha yao kutokana na kipato kilivyo.
Ukiangalia mavazi, usafiri na huku anataka
kuonekana kila sehemu ya starehe, sehemu ya pato hupotea huko na mwisho
wa siku hubakia kuwa na umaarufu wa maneno na sifa za mdomoni .
Biashara?
Wengi zimewashinda kutokana na ukweli kwamba
hawana uzoefu na tija katika biashara. Huanzisha miradi kwa kasi kwa
kushirikiana na watu, lakini huwa hawachukui muda kwani hujikuta
wakitolewa nje kutokana na matumizi yao makubwa kuliko kipato.
Sifa kubwa ya mfanyabiashara ambaye anasimama kama mchumi ni
kuzijua hesabu zake kwa umakini jambo ambalo wasanii wetu wa kizazi
kipya hawana.
Ukiachana na hilo, wengi wamekuwa wakitumiwa tu
majina yao katika maduka lakini ukija kwenye ukweli, maduka huwa si yao,
majina hayo hutumika kunufaisha biashara za watu na mwisho wa siku
ukweli huja kubainika.
Upo mfano wa msanii mmoja aliyewahi kuwa na Baa
maeneo ya Sinza, lakini ukweli ukaja kugundulika kwamba baa ilikuwa ni
ya mwanamke aliyekuwa na uhusiano naye, pale walipoachana ndiyo siri
ikavuja.
0 comments:
Post a Comment