Qatar yapata kiongozi mpya
07:46Qatar yapata kiongozi mpya
Qatar imepata kiongozi wake mpya, Sheikh
Tamim bin Hamad al-Thani, ambaye amechukuwa madaraka kutoka kwa baba
yake, tukio ambalo ni la nadra sana kwenye mataifa ya Kiarabu.
Saudi Arabia, taifa jirani, la kifalme na ambalo limeendelea na
utamaduni wa wafalme wake kuzeekea na kufia madarakani, limekuwa la
kwanza kutoa salamu za pongezi kwa kiongozi huyo kijana, mwenye umri wa
miaka 33 tu, likisema limefurahishwa na hatua hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Saudia, SPA, Mfalme Abdullah ametuma ujumbe maalum kwa Sheikh Tamim.
"Kwa niaba ya watu, Ufalme na serikali ya Saudi Arabia, tuna furaha ya
kukupongeza kwa dhati. Tuna imani utaendeleza safari ya baba yako na
juhudi zake za kulitumikia taifa la Qatar na watu wake na pia kuimarisha
mahusiano kati ya mataifa yetu mawili." Amesema Mfalme Abdullah.
Hatua iliyotangazwa leo na baba yake Sheikh Tamim, Amir Hamad bin
Khalifa al-Thani, inamaliza wiki kadhaa za uvumi. Licha ya kutokutoa
maelezo zaidi katika tangazo lake, wadadisi wanaamini kwamba Sheikh
Hamad, mwenye umri wa miaka 61, ana matatizo ya kiafya.
Sasa Sheikh Tamim, ambaye alisomea nchini Uingereza, ataanza utaratibu
wa kuunda serikali mpya ambayo wengine wanaamini itakuwa tafauti sana na
nyengine zenye mawaziri wengi wazee, miongoni mwa mataifa yanayoungwa
mkono na Magharibi.
Hapatarajiwi mageuzi ya kisera
Kiongozi wa Qatar aliyeondoka madarakani, Hamad bin Khalifa al-Thani.
Hata hivyo, kiongozi huyo anayechukua hatamu ya taifa lenye utajiri wa
mafuta na gesi na pia ushawishi wa kisiasa kwenye eneo hilo, hatarajiwi
kufanya mabadiliko yoyote ya haraka kwenye siasa za nje.
Wakosoaji wanaituhumu Qatar kutumia utajiri wake mkubwa kujijenga
kisiasa ndani ya eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, jambo ambalo
limechochea uasi na mabadiliko ya uongozi kwenye baadhi ya mataifa hayo.
0 comments:
Post a Comment