'IDD AZZAN HAUZI UNGA'
01:27Wakizungumza na Uwazi juzi Bamaga, Mwenge jijini Dar, wapiga kura hao kutokea CCM, walisema madai kwamba mbunge wao ni mfanyabiashara wa ‘unga’ yamewashangaza sana.
Walisema haiingii akilini hata kidogo kwa mtu ambaye amepata utajiri wake huku majirani wakimuona halafu aangushiwe kashfa ya kufanya biashara hiyo haramu.
“Sisi hapa (Magomeni Makanya) tunamjua Idd tangu zamani akiwa kijana mdogo. Alikuwa na teksi akiwa anaendesha mwenyewe, akaja akanunua ya pili.
“Mwaka 1986 aliziuza, akanunua daladala aina ya Costa, akawa anaendesha mwenyewe, tena ilikuwa inafanya safari za Pugu Kariakoo, akaja akanunua lori, akawa anaendesha mwenyewe,” alisema mzee Mussa, mkazi wa eneo hilo.
Naye Bakari au maarufu kwa jina la Jabu, alisema yeye anakumbuka mwaka 1986, mheshimiwa akiwa anasaka maisha alifanya biashara ya kupeleka redio Bujumbura nchini Burundi kisha anarudi na mashati yalikuwa maarufu kwa jina la Juliana, anauza Dar, tayari kipindi hicho Idd ana fedha zake.
“Sasa leo wanapozuka watu na kusema anauza dawa za kulevya, tunashangaa sana. Sisi majirani zake achilia mbali kuwa wapiga kura wake tungejua.
“Watu wanaojazana nyumbani kwake kabla hajaamua kuikarabati hii nyumba hapa wengi ni wale wenye matatizo, wanaomba msaada,” alisema mzee huyo.
Mzee mwingine, Hussein alisema anakumbuka mwaka 1989, yeye alikuwa shahidi wakati Azzan alipokopeshwa semi trela aina ya Mercedes Benz na kaka yake kwa makubaliano ya kumlipa fedha mwaka 1992.
“Azzan alikubali masharti hayo, akawa anaendesha mwenyewe kwenda nje ya nchi. Alikuwa akienda Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi mpaka Kongo.
“Na alikuwa akirudi anatubebea zawadi za chakula wazee wake kwa sababu ya ukaribu, mwaka elfu moja mia tisa na tisini na mbili alilipa deni, semi trela ikawa yake na akanunua jingine kama hilo.
“Nakumbuka kuna mwaka alipata ajali mbaya sana kule Ngara, akaumia na kulazwa, tukapata taarifa.
“Alipotoka akaamua kuanzisha Kampuni ya Azzan Investment na kununua mabasi mengi ya kukodisha, ndivyo ninavyojua mimi asili ya utajiri wa huyu bwana. Azzan hauzi unga bwana,” alisema mzee huyo.
Siku hiyohiyo, Uwazi lilimtafuta kwa simu Mheshimiwa Azzan na kumuuliza kama anawajua wazee hao ambapo alisema ni wazee wake anaowaheshimu sana, lakini akaomba asiongee kwa undani sana kwa vile alikuwa kikaoni.
Hivi karibuni, mtu mmoja aliyedai yupo jela Hong Kong, China kwa ishu ya unga aliandika majina ya watu aliodai ndiyo wafanyabiashara wa madawa ya kulevya na kuyatumbukiza majina hayo mtandaoni. Miongoni mwa majina hayo limo la Idd Azzan.
0 comments:
Post a Comment