ALIYEPELEKA VIDEO YA MKUU WA USALAMA WA CHADEMA AKIPANGA VITENDO VINAVYOSADIKIKA NI VYA KIGAIDI, NI HUYU HAPA

HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, amekiri kuhusika na video inayomwonesha Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.

Nchemba amekuwa akitajwa na viongozi wa CHADEMA kuwa anahusika kutengeneza video hiyo, kwa kuwa aliwahi kutamba wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni kuwa anayo video inayowaonesha viongozi wa chama hicho wakipanga mauaji.

Hata hivyo, tangu Nchemba atoe kauli hiyo Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi lilikaa kimya hadi Machi 12 lilipomkamata na kumhoji Lwakatare, siku moja baada ya video hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa You tube na mtu anayejiita ‘Bukoba Boy’.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Nchemba alikiri kuwa ndiye aliyeipeleka video ya Lwakatare polisi na kwamba alifanya hivyo baada ya kuripoti kuandikiwa ujumbe wa simu wa kutishiwa maisha na baadhi ya viongozi wa CHADEMA.

“Niliwapelekea mimi hiyo video polisi na wakati nasema kwenye televisheni nilikuwa tayari nimewapa. Na pale nilisema makusudi baada ya Zitto Kabwe kudai kuwa mwaka jana kulitokea mauaji mengi, ndipo nikataka kumuonesha kuwa chama chake kinahusika na mikakati hiyo,” alisema. Alipoulizwa aliipataje video hiyo na kwanini hajahojiwa polisi ili kutoa uthibitisho wa uhalali wake, Nchemba alisema: “Kuna msamaria mwema aliniletea.”

Nchemba alipobanwa ana uhakika gani kama video hiyo ina ukweli, alijibu kuwa: “Ile huhitaji akili kubwa kutambua uhalisia wake. Suala la Lwakatare CHADEMA wakubali tu na wajitokeze hadharani kwenye makanisa na misikiti, watubu na kuomba radhi kwa umma.”

Ndg wana JF sijashiriki kurekodi mkanda wa video unaomwonesha kiongoz mwandamizi wa CHADEMA akipanga mauaji ya mhariri wa gazeti. Mambo yako dhahiri kwani video inaonesha pale ni nyumbani kwake. Pili sikumtuma mtu akarekodi mkanda huo. Niliwahi kusema nina mkanda haina maana kuwa nilituma mtu.

Mikanda niliyokuwa nayo nilipewa na kiongozi wa CHADEMA anayechukizwa na vitendo hivyo vya kinyama. Ndugu zangu wa CHADEMA, najua nawakera na hampendi kusikia haya nawashauri msihangaikie habari ya Mwigulu ameshiriki bali hangaikieni kwanini kiongozi mwandamizi anafanya hayo pia kwanini anafanya kizembe mpaka mkanda unanaswa na tatu mjiulize. Kwangu mimi sioni kama kupata mkanda huo kwa kupewa au kwa hela ni dhambi kubwa kuliko ya kupanga mauaji.

Niwambie tu mkanda niliopewa sikuweka hata nukta na nilikabidhi vyombo vya usalama.

--- Mwigulu Nchemba via JF - Sijashiriki kurekodi mkanda wa video unaomwonesha ndg Lwakatare
Hata hivyo katika kile kinachoweza kuongeza mashaka ya Nchemba kuhusishwa kutengeneza video hiyo, alikwenda mbali zaidi akitoa hata siri za polisi, akisimulia maelezo aliyodai kuwa ndiyo yalitolewa na Lwakatare wakati akihojiwa na polisi.

“Pale video inaonesha ni nyumbani kwake, tena jikoni na hilo amekiri katika maelezo yake polisi. Pia amekubali kuwa
siku hiyo alipiga chafya kama inavyoonekana. Sasa wewe mwandishi unatetea nini wakati yeye amekiri polisi kila kitu kilichomo mle,” alisema.

Maelezo ya Nchemba yalionekana kumtia hofu mmoja wa mawakili wa Lwakatare, ambaye alikuwepo wakati wote wa mahojiano polisi, Nyaronyo Kicheere, akidai kuwa ni wazi jeshi hilo linafanya kazi ya propaganda za CCM.

“Nchemba hakuwepo wakati Lwakatare akihojiwa na hata baadhi ya wanasheria katika kesi yake ya ugaidi inayomkabili hawajui alichokisema polisi, sasa huyo amepata wapi siri za polisi kama si mchezo unachezwa?” alihoji.

Kuhusu mahusiano yake na mshtakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, Ludovick Joseph, ambaye anadaiwa na baadhi ya watu kuwa ndiye aliyerekodi video hiyo, Nchemba alisema walifahamiana kupitia mtandao wa kijamii wa facebook.