Msongamano wa magari chanzo cha maradhi ya akili, moyo


Wakati tatizo sugu la foleni likiendelea kuwaumiza wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake, utafiti mpya umebaini kuwa watu wanaokaa katika foleni mara kwa mara na kwa muda mrefu huweza kupata maradhi ya akili.
Imebainika kuwa foleni huchangia kwa kiasi kikubwa kusababisha maradhi ya akili yanayoweza kujitokeza baada ya miaka kumi, pamoja na ugonjwa wa moyo.
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Saikolojia na Tabia za Watu ya nchini Marekani, umebainisha kuwa kukaa katika msongamano wa magari kwa muda mrefu, husababisha mtu kunong’ona au kulalama, hatimaye kutoa sauti kwa kubwa.
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa pia na Mradi wa Maendeleo wa Marekani (MDM), ulijumuisha wanaume na wanawake wenye miaka 25 na 74.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia(NCCR) aliwahi kusema kuwa tatizo la msongamano wa magari hulisababishia taifa hasara ya takriban Sh1.46 trilioni kwa mwaka.
Ilibainika kuwa matatizo ya akili huweza kusababishwa pia na changamoto katika maisha, ikiwemo kukerwa au kuudhiwa katika misongamano ya magari.
Utafiti huo pia uliungwa mkono na Mtaalamu wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma Modester Kimonga, aliyesema kuwa kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu husababisha hasira, hatimaye msongo wa mawazo.
Alifafanua kwamba tatizo sugu la msongamano wa magari huchagiza maradhi ya moyo.
“Fikiria, unafanya kazi mbali na unapoishi na huwezi kuhama kwa kuwa umejenga huko. Mwajiri wako ni mkali. Kutokana na kuchelewa, ajira yako inakuwa mashakani. Matokeo yake siku zote utakuwa ni mtu wa kuogopa na mwisho wake unapata maradhi ya moyo,” alisema Kimonga.
Aliongeza kuwa foleni pia husababisha chuki baina ya wananchi na Serikali au wahusika wa Idara ya Usalama Barabarani.
Kimonga alifafanua kuwa kwa kawaida msongamano humfanya mwananchi wa kawaida aone kuwa Serikali haitekelezi majukumu yake, watu wa usalama barabarani nao huona wananchi ndiyo wanaovunja sheria.
“Inakuwa ni kama mchezo wa kutupiana lawama,” alisema Kimonga.