Video mtandaoni yawafungua Dayna, Kala Jeremiah, Kitale
23:46
Video iliyorekodiwa mjini Singida inayomwonyesha mwanamuziki
Mwanaisha Nyange maarufu kama Dayna akiwa chumbani na mwimbaji wa Hiphop
Kala Jeremiah iliyosambaa kwa kasi mtandaoni wiki hii, imezua mjadala
mzito kwa mashabiki wa muziki nchini.
Wakizungumza na Starehe kwa nyakati tofauti wanamuziki hao walisema hawakuwa katika hali ya kufanya mapenzi, bali walikuwa wakifanya usaili wa kuigiza filamu ya Mussa Kitale.
Kitale ambaye ni mwigizaji wa filamu na mwanamuziki anataka kuwashirikisha wanamuziki hao katika filamu yake mpya ambayo awali ilikuwa amshirikishe mwanamuziki na mwigizaji marehemu Sharomilionea. “Baada ya kufanya kazi kadhaa mkoani Singida ikiwamo shoo tulipumzika hotelini na baadaye tulizungumza na Kitale kuhusiana na uigizaji filamu, alihitaji tufanye majaribio,” alisema Dayna.
Alisema video hiyo ilirekodiwa na Kitale kupitia simu yake ya Android na baadaye aliirusha katika mtandao,
“Baada ya kurekodi aliirusha katika mtandao, lakini matokeo yake watu walivyoipokea ni tofauti pamoja na blogu mbalimbali kutoa taarifa zisizokamili,” alisema.
Kala Jeremiah alivyohojiwa na Starehe alisema video hiyo ilikuwa ni sehemu ya kipimo cha Kitale kwao kama wanaweza kuigiza hasa upande wa vichekesho.
“Watu wamepokea tofauti na taarifa zinatolewa tofauti, tulikuwa Singida wakati video hiyo inarekodiwa na Kitale ndiye aliyeshika simu yake na kuturekodi, dhima nzima ni usahili wa kucheza filamu ya Kitale,” alisema Kala Jeremiah.
Kwa upande wake, Kitale alipoulizwa alikiri kurusha mtandaoni video hiyo kwa madai kuwa alikuwa akiwaonyesha mashabiki namna wanamuziki hao walivyokuwa na vipaji vya kuigiza katika upande mwingine wa sanaa ya filamu.
“Kulikuwa na filamu niliyotaka kutengeneza na marehemu Sharomilionea, lakini kwa bahati mbaya ilishindikana baada ya yeye kufariki, nilirekodi mimi video hiyo na kuirusha katika mtandao wa kijamii nia ni kuonyesha ujio mpya wa wanamuziki hawa, walikuwa wanaigiza haikuwa kweli,” alisema Kitale.
0 comments:
Post a Comment