NAIBU WAZIRI WA ELIMU ATANGAZA KUWASHITAKI WANAODAI KUWA “AMEGUSHI VYETI”
23:11
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo amesema
atawafikisha mahakamani watu wanaodai kuwa ameghushi vyeti vya elimu ya
sekondari. Mulugo alisema amechoshwa na kashfa hizo zinazosambazwa na
baadhi ya watu atawafikisha mahakamani endapo wataendelea kumdhalilisha.
Mulugo alitoa kauli hiyo alipofungua mkutano wa mwaka wa Umoja wa
Wamiliki wa Shule za Sekondari na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO0)
jijini Mbeya.
“Wanasema eti nimeghushi vyeti, mara ooh sijui natumia jina la
mtu. Nimechoshwa na maneno haya… ni kweli nimerudia darasa kama
walivyorudia watu wengine, kwa nini iwe tatizo kwangu. Hata hapa tulipo
wapo wengi tu waliorudia darasa.
“Kama kweli ningekuwa nimeghushi vyeti hivi leo ningekuwa naibu
waziri wa elimu? Sasa nimechoshwa, nitawachukulia hatua watu hawa,
siwezi kusema ni lini nitafanya hivyo ila nitakapoamua nitaanza,”alisema.
Kwa miezi kadhaa sasa Mulugo amekuwa akidaiwa kughushi vyeti na
kutumia jina la mtu ili kufikia kiwango cha elimu alichonacho madai
ambayo alisema yanamchafulia jina katika jamii.
Kuhusu suala la matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana, Mulugo
alisema matokeo hayo mabaya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na
mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wanafunzi.
Naye Ruth Mnkeni kutoka Dar es Salaam anaripoti kuwa Mlugo
amezindua tovuti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari
ijulikanayo kama Shule Direct.
Muluigo alisema kuzinduliwa kwa tovuti hiyo kutawafanya wanafunzi
kupata maarifa mengi ya vitabu mbalimbali na kuinua kiwango cha elimu
nchini
0 comments:
Post a Comment