Kashfa nyingine ya kimapenzi yamwandama Prezzo

prezzo

KWA mara nyingine msanii wa humu nchini Prezzo amegonga vichwa vya habari kuhusiana na maisha ya kimapenzi.
Baada ya mpenzi wake wa Nigeria Goldie kufariki miezi michache,  msanii huyo mwenye mbwembwe nyingi akipendelea kutambulika kama ‘King wa mabling’ au ukipenda  ‘El Presindette’ amekuwa mbioni kujinasia mahabubwa mwingine.
Haikuchukua muda kabla ya mtangazaji mmoja wa radio nchini Tanzania kupasua mbarika na kuelezea kwamba alikuwa katika mapenzi na prezzo.
Kipusa huyo anayetambulika kama Diva ni  mtangazaji katika stesheni ya Cloulds FM iliyoko mjini Dar-es-Salaam. Kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii amekuwa akielezea kuhusu mapenzi yake na Prezzo na hata zaidi kuweka picha alizopiga akiwa pamoja na naye.
Nchini pia Prezzo amehusishwa sana kimapenzi na mwanamitindo Huddah Monroe ambaye alikuwa mwakilishi wa Kenya katika shindano la BBA 8 mwaka huu, mashindano aliyobanduliwa baada ya wiki moja pekee.
Aidha amehusishwa pia na msanii kipusa Victortia Kimani ambaye ni mdogo wake msanii Bamboo.
Victoria Kimani amegonga vichwa vya habari kwa wiki kadha sasa huku pia akihusishwa kimapenzi na kiungo wa Celtic na Harambee Stars Victor Mugubi Wanyama.
Wanyama alipohojiwa na NTV majumaa kadha kuhusiana na suala hili licha ya picha nyingi zilizoonyesha wawili hao wakiwa pamoja mara kwa mara, alidinda kulizungumzia.
Kukana
Huenda visa hivi ndivyo vimemfanya Diva kujitokeza kwenye blogi yake kuweka mambo bayana kuhusu uhusiano wake na Prezzo. Katika taarifa kwenye blogi hiyo Diva hakukana kuwa katika uhusiano na Prezzo na kusisitiza kwamba kilichoko kati yao, ni kati yao wenyewe.
Pia alisema kwamba hana tatizo ikiwa Prezzo atapenda kuwa na uhusiano na Huddah, Victoria Kimani au kipusa mwingine yeyote yule na kumtakia kila la kheri. Haya ndiyo aliyoyatundika kwenye Blogi.
“Ikiwa ana uhusiano na Huddah au Victoria Kimani au nani, kwangu mimi ni kumtakia kila la kheri. Baraka zangu tayari anazo. Ila ieleweke kwamba siwezi mchukia Prezzo kwa chochote kile. Wengi wanamzungumza vibaya kwa kuwa hawamwelewi. Ila kwangu yeye ni nguzo yangu na chanzo change cha furaha kila siku,”.
Credit: Swahili Hub