Mwanafunzi Chuo wa Kike Abakwa Na Kuuaua!

JoyceNjeriKagi

HUZUNI metanda eneo la Kikuyu baada ya mwili wa mwanamke wa umri wa miaka 19 kupatikana uchi na umedungwa mara mbili kwa kifaa chenye makali.
Chumba ambacho mwili wa Joyce Njeri Kagi ulipatikana kilikuwa kimeloa damu katika kiti na zulia, huku kuta na mlango zikiwa na alama za damu.
Runinga ilikuwa imeanguka chini na Bi Njeri alikuwa amepiga magoti akiwa uchi kando na kiti, na nguo zake katika kiti ambacho kilikuwa karibu naye.
Ripoti ya mkuu wa polisi eneo hilo, Joshua Opiyo ilithibitisha tukio hilo na pia kuwa mwili wa msichana huyo ulipatikana umedungwa kwenye shingo na kifua, ingawa jamaa wake walisema alikuwa amedungwa mara tano.
OCPD Opiyo aliongeza kuwa walimtia nguvuni mshukiwa, Thomas Olang, 24, ambaye alidai kuwa marehemu alimlazimisha yeye kufanya ngono naye kisha akajaribu kumdunga kwa kisu lakini yeye akajiokoa na badala yake kumuua yeye.
“Bado tunaendelea na uchunguzi lakini Bw Olang atafikishwa kortini siku ya Jumatatu kulingana na ushahidi  ambao tumepata,” alisema.
Polisi pia walipata kisu cha jikoni ambacho kilitumiwa kumuua msichana huyo, kikiwa kimetupwa kando ya barabara katika eneo la karibu na Kikuyu linaloitwa Ondiri.
Marehemu alikuwa anasoma Kijerumani katika chuo la Forrnax huko Nairobi na alikuwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne.
Mauaji haya inadhaniwa yalitekelezwa saa kumi na mbili jioni siku ya Ijumaa, kwani Binamuye marehemu Esther Muthoni aliporejea kutoka kazini saa moja unusu hivi alipata damu ilikuwa haijakauka.
“Nilishangaa kupata chumba kimefungwa kutoka nje ilihali sisi hufunga ndani,” alisema.
Maabara
“Nilipofungua mlango, niliona damu hapa na pale na binamu yangu amepiga magoti kando na kiti alichojishikilia akiwa uchi,” alisema Bi Muthoni.
Bi Muthoni ambaye hufanya kazi katika maabara hospitali ya St Theresa huko Kikuyu alisema kuwa alishangaa kupata vitu katika chumba vimetapakaa na jambo la kwanza alifanya ni kuangalia kama moyo wa binamuye ulikuwa unapiga kwa kugusa sehemu yake ya shingo.
Polisi walijulishwa kuhusu tukio hilo huku majirani na wapita njia wakifika mahali hapo kushuhudia kilichotokea.
Majirani walisema kuwa hawakusikia kelele yoyote kutoka chumba hicho kwani kulikuwa kunanyesha mvua kubwa.
Kakake marehemu, Laban Ndegwa alisema kuwa dadake alikuwa mtiifu na mwenye urafiki na alishangaa nani aliweza kumtendea unyama wa aina hiyo na kumtoa uhai.
Alisema, “Dadangu alikuwa na ndoto ya kufanya kazi ya uuguzi lakini sasa maisha yake yamekatizwa angali mchanga,” alisema Bw Ndegwa ambaye ni kifungua mimba katika familia hiyo.
Aliongeza kuwa familia ambayo inaishi kijiji cha Gituamba huko eneo bunge la Gatundu Kaskazini ilishangazwa sana na mauaji hayo na kuhuzunika.