Utata mkubwa bomu lililolipuka Arusha
00:18
Dar/mikoani. Mlipuko wa bomu uliotokea Arusha 
na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi 70 limezua utata 
kutokana na hisia tofauti za viongozi mbalimbali nchini waliozungumzia 
suala hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akisema haamini kama Watanzania 
sasa wamefikia hatua ya kuanza kuhasimiana kwa misingi ya kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha 
kushambuliwa kwa bomu baada  ya lile lililorushwa kwenye Kanisa la 
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi kwenye Parokia ya Olasiti wakati
 wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu na 
kujeruhi 64. Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema, 
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wamesema 
tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Kufuatia tukio hilo, uchaguzi wa  kata nne za Arusha mjini umeahirishwa hadi Juni 30.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa 
Rais Kikwete ambaye yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi 
zilivyoendelea kiviwanda(G8), alisema haamini kama Watanzania ama 
wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kudiriki kufanya 
matukio ambayo yanahatarisha usalama wa watu.
“Mimi   siamini   kuwa  Watanzania au wafuasi wa 
vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa 
aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema
 nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki 
miongoni mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye 
machafuko makubwa.”
Mbowe
Akizungumzia suala hilo,  Mbowe alisema shambulio 
hilo la bomu ni la kisiasa na lililenga kumuua yeye na Mbunge wa Jimbo 
la Arusha, Godbless Lema.
“Haya ni mauaji ya kisiasa ya kupanga, tumeokota 
maganda ya risasi za bastola na SMG na tumepiga picha na kuwapa polisi 
katika eneo la tukio, gari letu lilipigwa mlango na vioo kwa risasi na 
kesho wabunge wote wa Chadema watakuwa hapa Arusha na wataondoka baada 
ya mazishi,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema pia wamebaini bomu lililorushwa ni 
la kiwandani na shambulizi hilo liliandaliwa na kikosi cha watu wengi 
wenye lengo la kufanya mauaji makubwa.
Alisema kilichomwokoa na kifo ni kushuka jukwaani 
saa 11:43 kabla ya muda wa kawaida wa saa 12:00 kwani ilipangwa 
washambuliwe wakiwa juu ya jukwaa.
“Tunasikitika sana, watu wamekufa wasio na hatia 
na msiba huu utakuwa wa kitaifa na tunatarajia kuaga miili katika uwanja
 huohuo wa Soweto,” alisema Mbowe.
Profesa Lipumba
Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema watu waliohusika kulipua bomu walipanga kuvuruga uchaguzi huo uliyokuwa ufanyike jana.
Alisema CUF walikuwa na nguvu katika baadhi ya 
maeneo ya uchaguzi Arusha ndiyo mana watu wameamua kuvuruga uchaguzi  
ili usifanyike.
“Sisi tumewasimamisha wagombea udiwani ambao ni 
Abbas Mkindi, (Kaloleni), John Bayo (Elerai) na Labora Ndarvio (Themi) 
na maeneo haya tulitegemea leo (jana) tushinde ila baadhi ya watu 
wameamua kuvuruga kwa malengo yao binafsi,” alisema Lipumba.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amevitaka 
vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliohusika na 
milipuko hiyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi na Mwema
Wakati viongozi hao wakigawanyika Waziri wa Mambo 
ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi na Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP), Said 
Mwema wamesema tayari jeshi lake limetuma timu inayoongozwa na Kamishna 
wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna wa Idara ya 
Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Dk Nchimbi 
alisema uchunguzi wa awali umebaini ya kwamba bomu hilo ni la kurusha 
kwa mkono (hand grenade).
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema hadi sasa hakuna mtuhumiwa  yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
“Uchunguzi wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni 
la kutupa kwa mkono. Tunachunguza kujua mlipuko ule ni wa aina gani,” 
aliwaambia waandishi wa habari jijini  Arusha.
Dk Nchimbi alitaja orodha ya vifo katika tukio 
hilo na kusema hadi sasa watu wawili wamethibitishwa kufa, huku 70 
wakiwa wamejeruhiwa ambapo kati ya majeruhi hao, wawili wako katika hali
 mbaya. Alisema kwamba uchunguzi huo unalishirikisha Jeshi la Wananchi 
wa Tanzania (JWTZ) ili kubaini mlipuko uliojitokeza ni wa namna gani.
Naye IGP Mwema alisema jeshi litaendesha 
operesheni kali popote nchini ya kuwasaka na kuwatia mbaroni wote 
waliowezesha, kufadhili na waliotenda uhalifu huo. Alisema Jeshi la 
Polisi linalaani tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo 
limesababisha vifo na majeruhi pamoja na kujenga hofu kwa wananchi.
“Nawashukuru wananchi walioanza kutupa taarifa za mwonekano, wajihi wa mtu aliyetupa bomu hilo,” alisema.
Mwema aliweka hadharani simu yake ya mkononi yenye namba   0754 785557  akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
0754 785557  akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
 0754 785557  akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
0754 785557  akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando (Dar), Mussa Juma na Moses Mashalla (Arusha).

 
 
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment