MWINYI:”KILA MTU ANAHAKI YA KUCHINJA NA KULA CHOCHOTE HATA CHURA”…
05:53
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amerejea kauli
yake kuhusu mgogoro wa udini akisema kila mtu ana haki ya kuchinja
kutokana na imani yake ilimradi tu asivunje sheria za nchi.
Mwinyi alisema anashangaa kuona watu wakigombania kitu kidogo kama
kuchinja ilihali Tanzania ina utamaduni wa amani siku zote na kwamba
kila mtu ana imani yake ya dini anayoiamini.
Kiongozi huyo mstaafu alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam
katika kongamano juu ya utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki ambapo
Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji.
“Imani ni nafsi ya mtu na haitakiwi kumlazimisha kula nyama
iliyochinjwa na mwenzie. Na kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu
basi usile chinja yako, kula hata ukitaka kula chura, mjusi, konokono,
kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai,” alisema.
Mwinyi alikumbusha kuwa hata wakati wa utawala wake majaribu kama
hayo yaliwahi kumtokea, lakini alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia
kila mtu ale kile anachofikiri ni chakula bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema Watanzania wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni
kuwa na misingi ya kuvumiliana, na kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na
kuwa na uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu si kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na
makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya nchi kwa kutumia jina la dini ya
Kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu
Duniani (Rabita), Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki kwa kuichagua Tanzania
katika kuhubiri amani.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ambaye alimuwakilisha Makamu
wa Rais Dk. Gharib Bilal katika kongamano hilo, alisema kuwa utamaduni
wa Kiislamu Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla ni kuvumiliana katika
dini.
Pia aliwataka Waislamu kujiendeleza katika elimu, akisema kuwa hata
Mtume alihamasisha hayo, lakini Waislamu wameshindwa kuyafuata.
Prof. Maghembe alitoa mfano kuwa Waislamu wana Chuo Kikuu kimoja
wakati dhehebu moja la Lutherani lina vyuo vikuu 11, akisema ni vyema
wakaungana na kujenga vyuo kwa ajili ya kusaidia kuongeza wasomi katika
taaluma mbalimbali.
“Suala la elimu ya dunia pia ni muhimu, lakini mfano mzuri wa elimu
kushuka ni katika mikoa ya Pwani ambako ndiko ilipoanzia. Mathalani
mwaka 1995 wanafunzi walioanza darasa la kwanza walikuwa 35,000 lakini
waliomaliza darasa la saba ni 9,000. Hapa inaonesha Waislamu tunarudi
nyuma,” alisema.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki
alisema katika nchi ya Saudia wanaishi watu tofauti, lakini wakiwa
katika upendo huku akisisitiza kikubwa ni kuheshimiana.
Alisema Rabita imekuwa ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za
Nigeria, Gabon, Jamhuri ya Kongo na baada ya ziara yake nchini hapa
atahitimisha kwa kuitembelea Sudan.
Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania likiwa na lengo la kusisitiza amani nchini.
0 comments:
Post a Comment