Ripoti ya Polisi yamsafisha RC Mulongo dhidi ya Lema

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amedai uchunguzi wa awali kuhusu ujumbe unaodaiwa kutumwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo(pichani), umetumwa na mtandao wa simu wa nje ya nchi. Kamanda alisema katika ujumbe huo ambao Lema anadai uliandikwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo na kutumwa kwenye simu yake Aprili mwaka huu, uchunguzi wa polisi umeonyesha kwamba haukutumwa kupitia kampuni moja wapo ya simu za mikononi ya hapa nchini. 

“Katika kipindi cha mwishoni mwa Aprili mwaka huu, vyombo vya habari viliandika na kutangaza habari iliyoelezea shutuma zilizotolewa na Mbunge Lema kuwa aliandikiwa ujumbe wa vitisho kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa Mulongo na ulisomeka: “Umeruka kihunzi cha kwanza nitakuonyesha mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi inayoitaka mimi.”
Sabas alisema ujumbe huo ulidaiwa kutumwa kutoka namba 0752960276 inayotumiwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo kwenda kwenye namba 0764150747 inayotumiwa na Lema.
Alisema kufuatia tuhuma hizo, polisi walianza uchunguzi kwa kuzingatia kuwa Mulongo alikanusha kutuma ujumbe wa aina yo yote kwa Lema.
Alisema uchunguzi huo ulihusisha kampuni ya simu ambayo mtandao wake ulitumika katika utumaji wa ujumbe husika.
Alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha ujumbe huo mfupi hakikuwa kampuni ya simu husika (hakuitaja) kwa vile ‘Centre Number’ iliyotumika kutuma ujumbe huo mfupi wa maneno ni 44780200332, ambayo siyo ya mtandao wa kampuni husika bali ni ya mtandao ulio nje ya nchi.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kubaini chanzo cha ujumbe huo mfupi wa simu na mtu aliyehusika kutuma kuutuma ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.
Mvutano wa madai ya ujumbe huo wa simu kati ya Mulongo na Lema ulizuka mwishoni mwa Aprili mwaka huu, baada kutokea vurugu za wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, hali ambayo ilipelekea kufunguwa kwa muda chuo hicho.
Kabla ya kutokea kwa vurugu hizo, wanafunzi walikuwa wamesitisha masomo wakitaka kuandamana hadi kwa mkuu wa mkoa kulalamikia kuuawa kwa mwanafunzi mwenzao aliyechomwa kisu na watu wasiojulikana.
Lema alidaiwa na Mulongo kwamba alihusika kuwachochea wanafunzi ambao baadaye walimzomea mkuu wa mkoa wakati alipotaka kuzungumza nao.
Hali hiyo ilisababisha kuzuka kwa vurugu iliyopelekea polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutumia mabomu ya machozi.
Baada ya hapo Mulongo aliamrisha kukamatwa kwa Lema au la alitakiwa ajisalimishe, suala ambalo halifanyika.
Lema  alimtumu Mulongo kwa amri hiyo akielezea kuwa huo ni mwendelezo wa manyanyaso anayofanyiwa na mkuu huyo wa mkoa na akadai kuwa ametumiwa ujumbe huo na mkuu wa mkoa.
BY JOHN NGUNGE
SOURCE: NIPASHE