Sasa Obama kutua mwezi June, 2013
22:19
Ziara ya
siku nane ya Rais wa Marekani, Barak Obama na mkewe Michelle katika nchi
za Tanzania, Afrika Kusini na Senegal, imeelezwa kuwa ina lengo la
kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa
taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa
Afrika.
Wakati
wa ziara hiyo, itakayodumu kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, mwaka huu
Obama atakutana na viongozi mbalimbali wa kiserikali, sekta binafsi,
wafanyabiashara na jumuiya huru za kiraia ikiwamo vijana ili kujadili
ubia wa kimkakati katika ushirikano na masuala mengine ya kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu ya Marekani kuhusu ziara ya Rais
Obama barani Afrika na Ubalozi wa Marekani nchini kuisambaza katika
vyombo vya habari jana, ilisema ziara hiyo itadhihirisha dhamira ya
dhati ya Rais huyo kupanua na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi yake
na watu wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kuimarisha
amani na ustawi katika kanda hiyo na duniani kote.
Ilisema kuwa katika ziara yake hiyo, Rais Obama atawekea mkazo umuhimu
ambao Marekani inauweka katika ushirikiano wa kina na unaoendelea
kuimarika na nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mipango
mbalimbali ikiwamo ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na
biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika
kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika.
Ziara Rais Obama barani Afrika ni moja ya ahadi zake za kukuza na
kupanua ushirikiano kati ya watu wa Marekani na watu wa nchi za kusini
mwa Jangwa la SaharaAfrika katika masuala ya kimaendeleo na amani.
Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika. Ziara
yake ya kwanza aliifanya wakati wa awamu yake ya kwanza nchini Ghana.
Rais Obama alianza rasmi awamu yake ya kwanza kama Rais wa Marekani,
Januari 20, 2009 na awamu yake ya pili ilianza Januari 21, 2013.
Ziara ya Rais Obama inafanyika siku chache baada ya ziara ya Rais wa
China, Xi Jiping, ambaye aliyeitembelea Tanzania Machi 28, mwaka huu,
na Tanzania ilikuwa nchi yake ya kwanza kuitembelea barani Afrika tangu
achaguliwe kuwa rais, Machi 14, mwaka huu.
Baada ya ziara ya Tanzania, Jiping alikwenda Afrika Kusini kuhudhuria
mkutano wa mataifa ambayo uchumi wake unakua kwa kasi duniani.
Uchumi wa China unakua kwa kasi kubwa na hivi sasa taifa hilo linatajwa kuwa ni la pili kiuchumi duniani, baada ya Marekani.
China imekuwa ikitajwa kuwa inatafuta ushawishi katika mataifa ya Afrika
ili kupata rasilimali kama madini, mafuta, gesi na rasilimali
zitokanazo na misitu.
Ziara ya Obama inatazamwa kama njia ya kuendelea kujiimarisha barani
Afrika wakati China nayo ikiendeleza kusaka nafasi hiyo pia.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment